Mbunge wa CCM kuwajengea Nyumba Wajane wa Jimbo Lake

Mbunge wa Kibiti, Mhe Ally Seif Ungando yupo mbioni kuanza ujenzi wa nyumba za kudumu kwa wajane wote waishio wilayani Kibiti ambao waume zao wameuwa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa wakifanya mauaji kwa viongozi wa Serikali za vitongoji na vijiji, na wana Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza jana kwenye Ofisi za Mkuu wa Wilaya Kibiti alipokutana na viongozi wa Dini na wazee juu ya kufanya Kongamano la kuzidi kuiombea wilaya ya Kibiti iwe na amani, Ungando amesema mbali na kujenga nyumba hizo, pia atawasomesha watoto wote wa marehemu ambao wameuawa kwa kupigwa risasi kuanzia Mwezi May 2016 hadi sasa.
Amesema tayari ameanza kuwasiliana na wadau mbalimbali ili kumsaidia ujenzi huo kwa kuwa watu waliouawa hawakuwa na makosa yoyote.
Ungando, ambaye ameonekana kuguswa na mauaji hayo yaliyotokea mara kwa mara wilayani hapo kwa nyakati kadhaa alijikuta akitokwa na machozi katika mkutano huo hali iliyoelezwa na baadhi ya Wazee kuwa mauaji hayo yamemuumiza sana.
Mhe Ungando amesema kila alipokuwa akifika kwenye maziko ya viongozi wa Serikali za Mitaa au ya mwanachama wa chama cha Mapinduzi aliyeuawa kwa kupigwa risasi alikuwa akiumia sana moyoni mwake hali iliyomfanya kushindwa kuzungumza chochote kutokana na kuwa na machungu mengi moyoni mwake.
“Kila nilipokuwa nakwenda kwenye Msiba wa kiongozi wa Serikali za Mitaa au msiba wa mwanachama wa chama cha Mapinduzi na kwenye maeneo yalipotokea mauaji ya Polisi moyo wangu ulikuwa ukiumia hali iliyokuwa ikisababisha kushindwa kuzungumza”,amesema Mhe Ungando kwenye kikao hicho.
Akizungumza katika Kikao hicho Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Juma Mlindo amesema kwa sasa ni wakati muafaka kwa wananchi wote kushikamana pamoja na kuiombea dua wilaya hii irejee kwenye hali yake ya usalama na Utulivu pamoja na wilaya za Rufiji na Mkuranga.
Mlindo amesema wao kama viongozi wa Dini mara kadhaa wamekuwa wakiiombea wilaya hii Dua,ili Mwenyezi Mungu aweze kurejesha hali ya utulivu kama hapo awali.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com