Rais agawa ekari 1,000 za Gereza Kwa Raia

RAIS Uhuru Kenyatta akiwa katika kampeni zake Mjini Kitale akiomba wenyeji kumpigia kura aingie Ikulu kwa awamu ya pili ameamuru Jela la Kitale litoe ekari 1,000 za ardhi kwa wenyeji ili wapanue mji wao.
"Hatua hii inatokana na mapenzi yangu kwa wenyeji wa Mji wa Kitale na ambao ningetaka kuona wakiafikia malengo yao ya uwekezaji ndani ya mji mkubwa,” amesema Rais Kenyatta akihutubu Jumamosi.
Amesema kuwa kuanzia wiki ijayo, kabla ya Agosti 8, 2017 ambayo ni siku ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu hapa nchini, ekari hizo zitakuwa zimefanyiwa usoroveya na kupeanwa kwa wenyeji.
Haijulikani vipande vya ardhi ndani ya ekari hizo vitatolewa kwa njia gani; iwe ni kuchezewa kamari, kuuzwa au kupeanwa kwa nani,
haifahamiki. Ni jambo la kusubiriwa.
Rais amepigia debe mwaniaji wa ugavana kwa tiketi ya Jubilee Party, Maurice Kakai, akisema, “Huyu ndiye atakayewajibishwa jukumu la kupanga mji mpya wa Kitale na ulio na nafasi pana ya kuandaa nafasi za ajira kwa wenyeji.”
Amesema kuwa serikali yake haijatelekeza watu wa Trans-Nzoia na ambapo licha ya kupata asilimia 37.24 ya kura katika uchaguzi mkuu wa 2013, Rais amesema kuwa amebakia rafiki wa eneo hilo.
“Nilipoingia, nimehakikisha kuwa asilimia 95 ya wakazi wako na stima hapa Trans-Nzoia. Nimewapa Waziri wa Maji ambaye ni Eugene Wamalwa na bado kuna wengine wakuu ndani ya serikali yangu wa kutoka hapa,” amesema.
Vifaa vya hospitali
Ameongeza kuwa hospitali za Endebes na Kitale zimepata vifaa vya thamani ya Sh8 milioni na ambavyo vitawezesha eneo hilo kuhudumia wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
Ameahidi wenyeji kilomita 250 za lami katika utawala wake wa awamu ya pili, na pia apunguze gharama ya fatalaiza kutoka kiwango cha sasa cha Sh1,800 kwa kilo 50 hadi Sh1,200 kwa kipimo sawa.
Naibu wa Rais, William Ruto akiandamana na rais na pia Gavana wa Bungoma, Ken Lusaka pamoja na Wamalwa, amedai kuwa manifesto ya National Super Alliance (Nasa) yameandikwa na 'matapeli' wa rasilimali za taifa hili.
“Raila Odinga ni Yoshua bandia anayeelekeza Wakenya kwa Kanani bandia ambayo haina maziwa na asali bali ina mito ya busaa na chang’aa,” amesema Ruto akikejeli wapinzani wao wakuu ambao ni Raila Odinga wa ODM na Kalonzo Musyoka wa Wiper.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com