Ateketeza kwa Moto Nyumba ya Mwanaume Mwenzie wakigombania Mke

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 52 katika Kaunti ya Kirinyaga sasa hana nyumba ya kulala baada ya maskani yake kuteketezwa na mpinzani wake katika suala la mapenzi anayeaminika kumchukua mwanamke mwenye umri wa miaka 48.
Leonald Njagi alijipata katika mkasa huo wa moto baada ya George Mureithi kulipiza kisasi cha kimahaba.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa Mwea Mashariki, Kizito Mutolo, nyumba ya Njagi ilichomwa usiku wa kuamkia Jumamosi na Mureithi.
“Wawili hao wako na maneno. Kitendawili ni kuwa, Njagi ameoa mwanamke aliyekuwa awali ameolewa na Mureithi. Akiwa ndani ya mahaba ya Mureithi, alikuwa amejaliwa watoto wanne wa kati ya miaka 17 na minne na ambao amewaacha kwa Mureithi,” amesema Mutolo.
Alipojitoa kwa ndoa hiyo ya Mureithi, mwanamke huyo ambaye ametambuliwa kama Loise Wanjira alipatana na Njagi na baada ya
uchumba hapa na pale kiuzee mtaani, wakaafikiana wawe wakiishi pamoja kama bibi na bwana.
“Ni katika harakati hizo za uhamisho wa kimapenzi ambapo Mureithi alipata habari na ameonekana kuingiwa na hasira ambazo zimemwelekeza kuchoma nyumba ya Njagi katika kijiji cha Block, Karumandi,” akasema Mutolo.
Afisa huyo wa polisi amesema kuwa “hadi sasa mshukiwa wa ujambazi huo wa kumchomea mwenzake nyumba ametoweka kutoka nyumbani kwake.”
Alisema kuwa maafisa wa polisi bado wanamsaka na akipatikana atawajibishwa mkondo wa kisheria.
“Huyu mzee amekosea kwa kuchukua sheria mikononi mwake. Angefuata utaratibu wa kutatua mizozo ya ndoa katika afisi za kiutawala.
Angeandaa kikao cha wazee na hilo liwekwe mezani na lijadiliwe na suluhisho ipatikane. Kuamua kuvamia nyumba ya mwingine na
kuichoma ni uhalifu,” akasema.
Alisema kuwa maafisa wake hawamfuati Mureithi ili kumpa hongera ya kulipiza kisasi kwa njia hiyo, “bali tunamsaka ili awajibikie maamuzi yake mabaya kuhusu utatuzi wa mizozo ya kijamii.”
Alisema kuwa ni bahati kubwa kuwa “Mureithi hakutomboa kufanikisha lengo lake kuu ambalo lilikuwa ni kumwaangamiza bibi huyo pamoja na kipenzi chake kipya.”
Akasema: “Kabla ya kuchoma nyumba hiyo, aliitana akimtaka bibi huyo atoke nje na arejee kwake nyumbani, lakini alipokataa, akatia nyumba mafuta na kuichoma. Ni bahati kuu kuwa wawili hao walitorokea usalama wao kupitia kwa dirisha huku wakiiwacha nyumba yao kuteketea hadi kuwa jivu.”

chanzo: swahili hub


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com