Mauaji ya Polisi Kibiti, DC Awashukia Wauaji

Baada ya polisi trafiki wawili kuuawa hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Gulamhusein Kifu ametema cheche kwa kuwajia juu wauaji na wanaosita kuwataja wahalifu wanaoendeleza mauaji kwenye wilaya yake.

Kifu alisema hayo wakati akizungumza na wanahabari wetu waliomtembelea ofisini kwake siku moja baada ya kutokea kwa mauaji ya askari wawili wa kikosi cha usalama barabarani, Sajenti Salum na Konstebo Masola wiki iliyopita.

Alisema ana hakika kwa kushirikiana na wananchi mwisho wa watu hao wanaoua wenzao umefika. “Ombi langu ni kila mwananchi awe huru kufichua maovu haya, anaweza kutoa taarifa polisi au ofisini kwangu na jina lake litalindwa, hawa ni watu wabaya wasifichwe,” alisema.

Kifu alikiri wilaya hiyo kuwa na machafuko hayo lakini alisema hayapo Kibiti peke yake isipokuwa vyombo vya habari ndiyo vinasababisha paonekane ni sehemu isiyoingilika.

“Mbona nyinyi mmefika mpaka hapa, je pangekuwa hapaingiliki hata nyie si msingefika? Ni kweli mauaji yanatokea lakini siyo kiivyo inavyoandikwa, tukishirikiana na wananchi, tutamaliza haraka sana tatizo hili. Vyombo vya dola vipo na vinafanyakazi usiku na mchana,” alisema Kifu.

Akizungumzia askari waliouawa
Kibiti, kiongozi huyo wa wilaya alisema matukio hayo anawaachia jeshi la polisi kuyazungumzia lakini kwa upande wake akiwa ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani, anawataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa kuwataja wahusika kwenye ofisi yake au kwa jeshi la polisi ili kutokomeza mauaji hayo na watakaotoa siri majina yao yatalindwa.

ENEO LA TUKIO
Wanahabari wetu walifika eneo la tukio katika Kijiji cha Msafiri mita chache kabla ya kufika Bungu kutokea Kijiji cha Jaribu Mpakani na kujionea uhalifu uliofanywa na wahalifu hao ikiwa ni pamoja na kuondoa uhai wa askari hao.

UHARIBIFU WA MALI
Wanahabari wetu wakiwa eneo hilo walishuhudia uharibifu mkubwa wa mali uliofanywa eneo hilo sambamba na mauaji hayo ambapo walilichoma moto gari moja aina ya Suzuki Vitara na pikipiki aina ya Kawasaki ambapo hata namba za usajili hazikuweza kuonekana.

MUUZA MACHUNGWA
Akizungumza na wanahabari wetu mmoja wa mashuhuda ambaye ni muuza machungwa (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama), alisema yeye alikuwa mbali kidogo na eneo hilo kwani hufanya biashara:

“Wale jamaa walikuwa watatu wamepakizana mshikaki kwenye pikipiki na aliyekuwa na silaha alikuwa katikati, walipofika tu eneo lile, trafiki wa kike ndiye aliyeanza kuwaona na kuanza kukimbia huku akipiga mayowe akisema ‘jamani tunakufaaa…’

“Wale askari wenzake nao walianza kukimbia lakini wauaji walikuwa wameshawawahi, Sajenti Salum alikuwa akikimbilia kuelekea kwenye nyumba moja kama unaelekea Bungu lakini kabla hajafika alipigwa risasi nyingi za miguuni na kuangukia kwenye kichaka.
“Akiwa anagalagala chini walimpiga risasi nyingi za kichwani, hapa ndipo alipolala hebu angalia hizo damu zilivyotapakaa kwenye majani (alikuwa akiwaonesha waandishi wetu),” alisema muuza machungwa huyo aliyekuwa mita chache kutoka eneo la tukio hilo.

Akimzungumzia Konstebo Masola, shuhuda huyo alisema yeye hakuweza kufika mbali kwani ndiye waliyeanza kumfyatulia risasi baada ya kufika eneo hilo.
Aliongeza kuwa, wauaji hao baada ya kutekeleza mauaji hayo walirudi kama wanaenda Bungu na kukunja upande wa kushoto.

Credits: global publishers


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com