Kiapo Ikulu: "Mimi huwa siteui watu hivi hivi, huwa naangalia uwezo wa mtu" asema Rais

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Juni, 2017 amemuapisha Bibi Anna Elisha Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Bibi Anna Elisha Mghwira amejaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Saidi Meck Sadiki aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo.

Hafla ya kuapishwa kwa Bibi Anna Elisha Mghwira imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Akizungumza baada ya kumuapisha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Bibi Anna Elisha Mghwira kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuondoa kero zinazowakabili wananchi wa Kilimanjaro bila kujali itikadi za vyama vyao vya siasa, dini, makabilia na kanda wanazotoka.

Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa atapata ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake na asikubali kuyumbishwa na mtu yeyote katika majukumu yake ya kuwahudumia wananchi.

“Mimi huwa siteui watu hivi hivi, huwa naangalia uwezo wa mtu, na wewe nimekuchunguza na nimejiridhisha kuwa una uwezo wa kuwatumikia wananchi, nenda kachape kazi, kawaondolee kero wananchi wa Kilimanjaro, wapo watu watakaokusema na wengine watakuonea wivu, wewe kachape kazi” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Bibi Anna Elisha Mghwira amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na amemuahidi kuwa yupo tayari kwenda kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi na kujenga Taifa.

“Ninasema hii ni heshima kwa Taifa letu, ni heshima kwa umoja wa nchi yetu, ni heshima kwa siasa za umoja wa nchi yetu, kumekuwa na minong’ono mingi sana kuwa Rais analeta nini, kuteua watu wanaitwa wapinzani, mimi sio mpinzani wa maendeleo” amesema Bibi Mghwira. 


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com