Wahudumu wa Mochwari wapasua Maiti, Watoa Dawa za kulevya na Kuziuza

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watuhumiwa wanne wa dawa za kulevya katika Hospitali ya Mwananyamala kwa kosa la kupasua mwili wa raia wa nchi ya Ghana aliyehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti (Mochwari) hospitalini hapo tangu alipofariki dunia Machi 14, 2017 kutokana na kumeza dawa hizo, kwenye nyumba ya kulala wageni ‘Red Carpet’ iliyoko maeneo ya Sinza.
Akifafanua tukio hilo lililotokea Mei 20, 2017, Kamishna wa Kanda hiyo Kamanda Simon Sirro ameeleza kuwa, wawili kati ya watuhumiwa hao ambao ni wahudumu katika mochwari ya Mwananyamala, Omary Rukola na Athuman Mgonja baada ya kuhojiwa na polisi walikiri kuuchana mwili wa marehemu na kuchukua kete 32 za dawa ya kulevya na kuziuza kwa Omary Wagile ambaye ni mtuhumiwa wa tatu.
Kamanda Sirro amesema baada ya Wagile kuuziwa kete hizo 32 za dawa za kulevya, alimuuzia Ally Nyundo ambaye pia ana kesi nyingine ya utumiaji dawa hizo mahakamani.   
“Kupitia kikosi kazi kinachoshughulika na watu wanaojihusisha na biashara haramu ya usambazaji na utumiaji dawa za kulevya, jeshi la polisi lilifanikiwa kukamata watuhumiwa wanne wa dawa za kulevya baada ya kuwepo kwa taarifa ya kupokelewa kwa mwili wa marehemu aliyefariki kutokana na kumeza dawa za kulevya, wahudumu wa mochwari wawili walikiri kufanya upasuaji,” amesema.
Amesema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na uchunguzi zaidi utakapo kamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Kuhusu mwili wa marehemu amesema Jeshi la Polisi litawasiliana na Ubalozi wa Ghana ulioko nchini Kenya kwa ajili ya kutafuta ndugu wa marehemu.
Katika tukio lingine, Kamanda Sirro amesema Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa mmoja aitwaye James Washokera (24) kwa kosa la kukutwa na bastola aina ya Browining ikiwa na risasi 2 .
Amesema baada ya mahojiano mtuhumiwa hiyo alikiri kumiliki silaha hiyo isivyo halali, baada ya kuiiba kwa Afisa Misitu Nurdin Samuya maeneo ya Ukonga Kichangani.

Na Regina Mkonde


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com