Wabunge ‘Wamlilia’ Halima Mdee Bungeni

DODOMA: WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali itikadi ya vyama vyao, wameungana kwa kauli moja leo Mei 2, 2017 na wamekubali Mbunge mwenzao, Halima James Mdee wa Kawe (Chadema) asamehewe kutokana na kosa la kutoa lugha isiyo na staha kwa Spika Job Ndugai.
Mapema leo asubuhi Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ilitoa uamuzi wake wa kumsimamisha asihudhurie vikao vyote vya Bunge vilivyobakia kutokana na kosa hilo.
Mdee na Freeman Mbowe walijitokeza mbele ya Kamati ya Maadili kujibu tuhuma za kutoa lugha isiyokuwa na staha kwa Spika Job Ndugai bungeni siku ya uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Aprili 5, mwaka huu.
Baada ya Mdee kusimamishwa, huku wabunge wengine na viongozi wa mikoa na wilaya waliokuwa na makosa kama hayo wakisamehewa, wabunge walianzisha mjadala wa kumtetea wakitaka asamehewe kwani aliomba msamaha Bungeni mbele ya wabunge wote wiki iliyopita huku akiahidi kutorudia kosa.
Baada ya mvutano wa muda mrefu, wabunge wote wameridhia Mdee asamehewe na kumuonya asirudie kosa tena.
Akisoma maazimio ya Bunge kuhusu mjadala huo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Joakim Mhagama amesema kuwa, Bunge kwa kauli moja limemsamehe Halima Mdee, hivyo adhabu yake ya kutohudhuria vikao vya bunge vilivyobaki imefutwa.
Aidha Bunge limempa sharti moja kuwa asirudie tena kutenda kosa kama hilo la kudharau kiti cha spika na endapo atarudia, basi atapewa adhabu kubwa zaidi tena bila kuitisha kikao cha kamati yoyote ya Bunge.
Pia Kamati hiyo, imemsamehe Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) kutokana na kosa la kutoa lugha isiyokuwa na staha mitandaoni kwa kuingilia Haki, Uhuru na Madaraka ya Bunge.
Kamati imefikia hatua hiyo baada ya Mbowe kukiri kosa hilo na kuomba radhi wakati alipohojiwa na kamati hiyo mjini Dodoma.
Mwingine aliyesamehewa ni Mbunge Ester Bulaya wa Bunda Mjini baada ya kupewa karipio kali na Kamati hiyo kutokana na kosa la kudharau Mamlaka ya Bunge.
Kamati pia imemsamehe DC Alexander Mnyeti kutokana na kukiri, kujutia kosa lake na kuliomba radhi Bunge.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com