Shoti ya Umeme yakatisha uhai wa Mama, Mtoto anusurika

Mama mmoja mwenye umri wa miaka 35 amefariki dunia papo hapo huku mtoto wake mwenye akinusurika baada ya mama yake kunasa na shoti ya umeme.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja  Suleiman Hassan Suleiman amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amesema kuwa Tukio hilo limetokea jana majira ya saa tisa na dakika arobaini jioni huko Bumbwini bondeni Wilaya ya kaskazini B.
Kaimu Kamanda amemtaja Marehemu kuwa ni Taifa Mohamed Ali mkazi wa Bumbwini bondeni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kabla ya kifo chake Marehemu alikua nyumbani kwake ambapo baada ya kumaliza kupika na kuanza kula inasadikiwa alikwenda kuufunga mlango wa geti huku waya wa umeme ulioko chini ya geti hilo ukiwa umechunika ngozi ndipo alipopigwa shoti na kunasa na kusababisha kifo chake.
Mtoto aliyenusurika kufa ametambulika kwa jina la Ali Mohammed Ali mwenye umri wa miaka 3 mkazi wa Bumbwini. Tayari mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Mnazi mmoja na kukabidhiwa ndugu zake kwa mazishi.

Andika maoni yako hapa (MATUSI HAPANA) 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com