Polepole: Watu wanaishi kwa hofu Kibiti


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amefunguka na kusema watu wamekuwa na hofu huku wengine wakihama makazi yao mkoani Pwani kutokana na vitendo vya mauaji vinavyoendelea mkoani humo.

Polepole amesema wao kama CCM wanaitaka serikali ichukue hatua za haraka katika jambo hilo kwa kuwa ina vyombo vyote vya ulinzi na usalama, hivyo wanataka kuona jambo hilo linapewa umaalum katika kulishugulikia.

"Sisi kama chama tumelifuatilia hili suala kwa umakini sana na tumeona ni vyema kusimama na Watanzania wakiwepo na wanachama wa CCM wa maeneo haya, tunatambua wanapitia wakati mgumu sana kwani wapo viongozi wetu, wapo wanachama wa CCM, na watendaji mbalimbali wamepoteza maisha. Wamepoteza maisha si kwa sababu ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu bali maisha yao yamekatizwa kikatili" alisisitiza Polepole

Kufuatia mambo haya kuendelea kutokea mkoani Pwani Chama Cha Mapinduzi kimetoa salamu za pole kwa wananchi wote ambao wameguswa na misiba ya watu ambao wameuawa lakini pia kimetoa rai kwa serikali kufanya mambo yafuatayo.

"Kupitia kwenu nataka nitoe rai kubwa kabisa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa tumevumilia, tumekaa kimya, tumefuatilia tena na tena lakini Watanzania wenzetu wameendelea kupotea, tunataka kuona kitu kinatokea ambacho kitarudisha amani. Watu wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji ni Watanzania kweli kweli kama sisi wengine, tunataka kuona kitu kinatokea, sisi ni taifa lenye heshima kubwa, linalofuata sheria na Katiba tunataka kinachotokea kiturejeshee amani. Watu wanaishi kwa hofu wengine wamekimbia nyumba zao CCM kinataka kuona kitu kinatokea Mkuranga, Kibiti na Rufiji" alisistiza Polepole wakati akizungumza na waandishi wa habari, Jijini dar es Salaam leo.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com