Mwanzo mwisho jinsi ajali ilivyotokea Karatu Arusha na Kuua wanafunzi 32

SIMANZI na vilio vilitawala eneo la Shule ya Awali na Msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent iliyoko Kwa Mrombo jijini hapa jana, baada ya wanafunzi 30, walimu wawili na dereva mmoja wa shule hiyo kufariki dunia kwenye ajali ya gari asubuhi.

Wakati hali hiyo ikitokea, majeruhi watatu ambao kati yao wawili ni wanafunzi, walipokewa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, wakitokea Hospitali Teule ya Karatu majira ya saa 9:45 alasiri jana.

Wazazi waliofika shuleni hapo walionekana mara kwa mara wakifuta machozi kwa kutumia vitambaa na kanga walizojifunga, wakati mama mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja akianguka na kuzirai.

Baadhi ya wanafunzi na walimu walionekana wakiwa wamesimama makundi makundi kwenye korido na uwanja wa shule, wakiwa na simanzi na huku wengine wakilia.

Mapema, majira ya asubuhi baada ya taarifa za ajali hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, mamia ya wakazi wa hapa wakiwemo wazazi walimiminika kwa wingi shuleni hapo kupata taarifa kamili.

Hata hivyo, hamu ya kujua kama miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo ni watoto wao iligonga mwamba hivyo kuwafanya kuanza kuangua vilio na kwa kadri muda ulivyozidi kwenda, idadi ya watu waliokuwa wakifika shuleni hapo ilizidi kuongezeka.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro, ambaye alifika shuleni hapo, alilazimika kutoa neno la pole kwa wazazi akisema serikali inaungana nao.

“Poleni kwa msiba huu. Nimekuja kama kiongozi wa serikali na binafsi kuungana na wazazi pamoja na shule kuomboleza msiba huu mzito," alisema.

"Hata hivyo, pole za Daqarro hazikuwazuia wazazi na majirani kuangua vilio hasa kutokana na vifo hivyo kuacha mapengo ya maisha.

“Serikali itatoa taarifa ya tukio hili baadaye… tusibiri taarifa ya mwisho na sahihi kutoka serikalini. Ninawaombeni tuwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu,” alisema.

Alisema serikali ilishaandaa utaratibu wa kusafirisha miili ya wanafunzi na walimu kutoka wilayani Karatu hadi Mount Meru ambako ingehifadhiwa katika chumba cha maiti.

Wengi waliokuwa wakilia hawakuwa wakijua kwa uhakika iwapo watoto wao ni miongoni mwa waliofariki au la, lakini wengine walilia kutokana na uchungu na kuhuzunishwa na tukio hilo.

AJALI ILIVYOTOKEA
Meneja wa Shule hiyo, Casmir Moshi alisema ajali hiyo ilitokea eneo la Malera wilayani Karatu, majira ya saa tatu asubuhi wakati mvua ikinyesha, baada ya gari kushindwa kufunga breki, kuserereka na kutumbukia kwenye korongo.

Wanafunzi waliofariki dunia walikuwa kwenye gari aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T871 BYS, mali ya shule hiyo.

Wanafunzi hao pamoja na wengine waliokuwa katika magari mengine mawili, walipelekwa wilayani Karatu kufanya mitihani ya pamoja ya kujipima na shule rafiki ya Tumaini Junior, utaratibu ambao huwa wanafanya kila mwaka kwa wanafunzi wa darasa la saba.

“Walisafiri katika mabasi matatu ya shule kwenda Karatu ambako walitarajiwa kufanya mitihani ya pamoja leo (jana) na wangerudi hapa baada ya mitihani yao," alisema.

Alisema tukio hili ni baya na kubwa kutokea katika shule hiyo ya bweni na kutwa yenye wanafunzi wengi kutoka Mkoa wa Arusha na jirani na hata kutoka Dar es Salaam, tangu ilipoanzishwa mwaka 2006.

Miongoni mwa waliokufa alisema ni dereva aliyemtaja kwa jina la Dismas Kessy na walimu wawili ambao hakutaja majina yao.

Wakati baadhi ya wazazi wakiwa shuleni hapo, wengine walikwenda moja kwa moja Mount Meru kusubiri kuona miili ya watoto na ndugu zao na pengine kupata uhakika wa hali za watoto wao au watoto wa ndugu zao.

Diwani wa Olasiti, Alex Marti na Mratibu wa Elimu Kata ya Olasiti, Joram Mringo, walisema wamehuzunishwa na ajali hiyo iliyoua wanafunzi.

“Nimeamua kuja hapa kuungana na uongozi wa shule katika maombolezo hayo kwa sababu shule hii ipo katika eneo langu la kazi,” alisema Joram.


MZAZI ASIMULIA
Mmoja wa wazazi, Tito Mau alisema watoto wao waliaga kuwa wanakwenda Shule ya Tumaini Junior kufanya mitihani ya pamoja ya majaribio.


Hata hivyo, alisema ilipofika saa 3:30 asubuhi, alipokea simu kuarifiwa kuwa kuna ajali imetokea inayowahusu wanafunzi hao.

Mzazi huyo ni miongoni mwa wazazi wengine waliofika hospitali ya Mount Meru a kusubiri taarifa za ajali hiyo.

RAIS MAGUFULI


Rais John Magufuli alisema ajali hiyo imezima ndoto za watoto hao waliokuwa wakijiandaa kulitumikia taifa.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Magudui alisema ajali hiyo imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na taifa kwa ujumla.

Katika taarifa hiyo Rais Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na kumweleza “Naomba unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha."


“Hiki ni kipindi kigumu kwetu sote na uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi.
“Muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.”


Aidha, Rais amemweleza kuwa amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi hao.

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, katika salamu zake za rambirambi amewaomba Watanzania wasimame kwa pamoja kusaidia jambo lolote litakalotakiwa kufanywa kutokana na msiba huo.

“Nimepokea kwa masikitiko tukio hili," alisema Lowassa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
"Ni ajali inayofanya siku hii kuwa mbaya katika historia ya nchi yetu, (na) nawapa pole wote waliofikwa na msiba huu.”

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba naye aliandika kwenye ukurusa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook akitoa "pole kwa familia, ndugu, jamaa na shule ya Lucky Vincent kwa msiba mzito huu uliolipata taifa letu uliotokana na ajali mbaya pale Karatu.


Tumepoteza watoto wetu ambao wazazi wao, ndugu zao na taifa kwa ujumla liliwategemea.
“Kwa kuwa Mungu wetu anaishi na kumiliki,tuendelee kuziombea familia zilizoguswa na msiba huu, watoto wetu wapumzike kwa Amani.”


Naye Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, katika taarifa yake, alisema taifa limepoteza nguvu kazi ambayo si rahisi pengo lake kuzibwa.

Pia ilisema chama chake kimepokea kwa majonzi na simanzi taarifa hiyo na kuwaombea kwa Mungu majeruhi wapone haraka ili waweze kuendelea na masomo yao mpaka watimize malengo waliyotarajiwa.


SPIKA AWALILIA
Wakati huo huo, spika wa Bunge, Job Ndugai, amemtumia salamu za rambirambi Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kutokana na ajali hiyo.


Katika salamu hizo, Ndugai alisema: “Nimepokea kwa mshtuko taarifa hii ya ajali iliyogharimu maisha ya watoto wetu. Hakika hili ni pigo kwa taifa zima. Namwomba Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.”

“Natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao, Mwenyezi Mungu awape nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu. Vile vile nawaombea majeruhi wote wa ajali hiyo wapate uponyaji wa haraka” aliongeza.

* Imeandikwa na John Ngunge na Cynthia Mwilolezi, ARUSHA na Romana Malya, DAR


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com