Muuaji sugu afunguka, aelezea mkakati wa kuwaua watu


Majyambere Bertin amekiri kuwa muuaji sugu na kuelezea waandishi wa habari mkakati wa mauaji ya watu walau elfu moja
Jeshi la Polisi la Rwanda linawashikilia wanaume watatu na mwanamke mmoja wanaodaiwa kutekeleza mauaji, ambapo mmoja wao amekiri kuwa muuaji sugu.
Wanne hao wamehusishwa na mauaji ya Iribagiza Christine yaliyofanyika Aprili 13, 2017 ambapo walimuua mida ya asubuhi akiwa nyumbani kwake katika Tarafa ya Niboye, Kicukiro.
Bw Majyambere Bertin amewataja watu lukuki aliowaua akiwemo marehemu Iribagiza na kuelezea mkakati aliokuwa nao wa kuua watu walau elfu moja.
Bw Majyambere alimuua Bi Iribagiza siku nne tu tangu atoke jela ambapo alikuwa anatumikia kifungo alichohukumiwa baada ya kumuua mdogo wake.
Aliporudi uraiani alikuta mali zake zote zinamilikwa na watu wengine akawa hata hana pa kuishi, ikabidi aamue kuanza kuwaua watu ili awapore mali zao, kwa mujibu wa maelezo yake.
Ili kufanikisha shughuli ya kumuua Bi Iribagiza, Majyambere alimshirikisha Bwana Hatungineza Hassan ambaye walifungwa wote kwenye Gereza la Gasabo lililoko mjini Kigali.
Waliingia kwa marehemu Iribagiza wakiwa na mke wa Hatungineza, wakiwa wamejifanya wapelelezi wa makosa ya jinai. Mlinda geti walimdunga visu alipowakataza kuingia nyumbani.
Walipoingia nyumbani wakamlazimisha Bi Iribagiza kuwapa kitita cha faranga miliyoni 25, akawabishia. Hapo ndipo wakamnyonga kwa kutumia shuka, kwa mujibu wa maelezo yao.
Baada ya utekelezaji wa mauaji hayo, haikuishia hapo kwani walimuua hata mlinzi wa geti aitwaye Fabrice sehemu za Gacuriro wilayani Gasabo ili waweze kuiba televisheni.

Baadhi ya televisheni walizoiba Gacuriro baada ya kumuua mlinzi

Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Théos Badege amesema baada ya mauaji ya Bi Iribagiza, walianza upelelezi na kuja kubaini kuwa mauaji hayo yana fungamano na mauaji ya Gacuriro.
Majyambere anayekiri kuwa muuaji sugu aliwaambia waandishi wa habari kuwa hata siku hiyo hiyo ya Jumamosi aliyoongea nao, alikuwa amuue mtu, bahati mbaya akawa ameshakamatwa.
Msemaji wa Polisi, ACP Badege amesema wanaume hao wamekuwa wakiwatumia wanawake waendako kufanya mauaji wakiwa wamejifanya wapelelezi ili wasishukiwe kuwa wahalifu.
Washukiwa hao walio mikononi mwa polisi wanakabiliwa na makosa matatu ambayo ni pamoja na mauaji, kuunda genge la uhalifu na wizi.

Majyambere, Hatungineza na mkewe, na mwendesha pikipiki aliyewapeleka Gacuriro walikoiba televisheni baada ya kumuua mlinzi wa geti.

Polisi wanadai wana imani kuwa washukiwa watatiwa hatiani kwa misingi ya ushahidi toshelevu uliopo dhidi yao.
“Ninaamini waendesha mashtaka watashinda kesi, na endapo washtakiwa watatiwa hatiani watahukumiwa kifungo cha maisha jela,” amesema ACP Badege.

ACP Badege amewashukuru raia waliotoa taarifa polisi katika juhudi za kufanikisha ukamatwaji wa washukiwa hao, na kuwasihi raia waendeleze ushirikiano na polisi katika kuzuia uhalifu.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com