Kamanda Sirro Amjibu Sheikh Ponda, ni kuhusu Kifo cha Salum

Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro amewataka watu wanaolalamika juu ya kifo cha Salum Mohamed Almas aliyeuawa hivi karibuni kwa tuhuma za ujambazi, kurudi katika eneo la tukio, wakachunguze kilichotokea, ikiwemo kuuliza wananchi waliokuwepo siku ya tukio kwa ajili ya kupata ukweli. 
Tukio hilo lilitokea Mei 14, 2017 majira ya asubuhi maeneo ya Kurasini katika jengo la Makao Makuu ya Uhamiaji, ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mei 15 mwaka huu, inasema marehemu huyo aliuawa wakati akijaribu kupora fedha za benki ya CRDB zilizokuwa zinasambazwa na gari la kampuni ya G4S katika mashine zake za kutolea fedha, huku majambazi watatu  waliokuwa katika pikipiki mbili wakikimbia kusikojulikana.
Kamanda Sirro ametoa ufafanuzi wa tukio hilo, leo Mei 22, 2017 baada ya Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa na familia ya Salum Mohamed Almas, kulalamika kuwa kijana huyo aliuawa kimakosa na kwamba alikuwa raia mwema. 
“Kuna malalamiko kwamba kijana aliyeuawa akidhaniwa ni jambazi alikuwa mwanafunzi mzuri na anafundisha madrasa. Lakini mtoto hawezi akamwambia mzazi wake kama ni mhalifu, vile vile kuwa mwalimu wa madrasa hakumaanishi kama huwezi kuwa mhalifu,” amesema na kuongeza.
“Yale maeneo yanafahamika, na zile fedha zilikuwepo, wanaotaka ushahidi waende kwenye tukio wakachunguze kilichotokea.”
Aidha kwa mujibu wa Sheikh Ponda kupitia barua yake aliyomwandikia hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, inadai kuwa Marehemu Salumu ambaye ni Mzaliwa wa Kilwa, alikuwa Imamu Msaidizi katika moja ya Misikiti Kurasini na alikuwa akishiriki ibada miskitini ipasavyo. Pia alikuwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ngazi ya Diploma.
 Na Regina Mkonde


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com