Binti Afariki Ghafla baada ya kuingia Gesti na Mwanaume Wake

DAR ES SALAAM: Tutakukumbuka daima! Ndivyo waombolezaji wengi walivyosikika wakisema kwa masikitiko kufuatia kifo cha mdada aliyefahamika kwa jina la Sophia William almaarufu Sophie kilichomkuta ghafla akiwa na mwanaume ambaye ni mpenzi wake kwenye chumba cha gesti na kuibua utata mkubwa, Wikienda lina habari ya kusikitisha.
Kwa mujibu wa vyanzo visivyo na shaka, tukio hilo lilijiri wiki iliyopita kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni ya Twiga iliyopo Keko-Juu jijini Dar ambapo Sophie alikuwa na mpenzi wake huyo aliyetajwa kwa jina moja la Haule.
Habari hizo za uhakika zilieleza kuwa, Sophie aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Ndege la Fly Emirates alifia kwenye gesti hiyo baada ya kwenda kujipumzisha na Haule na kwamba ni sehemu waliyoizoea.
Kufuatia tukio hilo, wanahabari wetu walifika kwenye gesti hiyo na kumkuta meneja msaidizi aliyejitambulisha kwa jina la Rajabu Mohammed aliyekuwa na haya ya kusema juu ya mkasa huo:
“Ni kweli tukio limetokea hapa kwenye ofisi yangu, lakini sina mengi ya kueleza, nafikiri mengi mtayapata polisi.
“Ninachoweza kusema ni kwamba ilikuwa majira ya saa nane usiku, Sophie na Haule walifika hapa na kuomba chumba kama kawaida.
WAPEWA CHUMBA NAMBA 105
“Ni watu ambao tunawafahamu kwa sababu siyo mara ya kwanza kuja kulala hapa, kwa hiyo licha ya kuja muda huo, tuliwafungulia na kuwapa chumba namba 105.
“Walilala hadi asubuhi, ulipofika muda wa saa tatu, Haule alikuja kutuambia anamshangaa mwenzake kwani haamki hivyo twende tukamsaidie kumuangalia ikiwezekana tumkimbize hospitali.
“Baada ya kutuambia hivyo, tulikwenda chumbani kumwangalia huyo mpenzi wake, lakini hatukuweza kuelewa kama alikuwa mzima au amekufa hivyo tukamuambia kwa inavyoonekana tusimpeleke popote bila kuwajulisha polisi.
POLISI WAITWA
“Tuliwaita polisi ambao nao walipofika, hawakuweza kupata uthibitisho wa moja kwa moja kama yu hai au amekufa.
“Ilibidi polisi watuchukue sisi wafanyakazi, Haule na mwili huo hadi Kituo cha Polisi cha Chang’ombe (Dar) na kutuchukua maelezo.
“Baada ya hapo waliupeleka mwili huo Hospitali ya Polisi ya Kilwa Road (Baracks).
“Daktari aliyeupokea mwili wa Sophie alisema tayari ameaga dunia.
“Baada ya kubainika hivyo, Haule anaendelea kushikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na sisi wafanyakazi tuliambiwa tukaendelee na kazi tutakapohitajika tutaitwa,” alisema meneja huyo.
Baada ya kuzungumza na meneja huyo, gazeti hili lilifika nyumbani kwa baba mdogo wa Sophie maeneo ya Sinza-Lion jijini Dar ambapo lilizungumza na mmoja wa ndugu ambaye alikataa jina kuandikwa gazetini:
“Ukweli tumepata pigo kubwa sana hasa kutokana na mazingira ya kifo chenyewe, tulikuwa tukihangaikia kuupata mwili wa marehemu ili tupange mazishi, lakini tunashukuru polisi wameshatukabidhi hivyo uko chini yetu na hapa ndiyo tunapanga tumzikie hapa Dar au Musoma ambapo ndipo tulimzika baba yake mwezi Machi, mwaka huu.”
UTATA WAIBUKA
Wakati taratibu za mazishi zikiendelea, ghafla kuliibuka juu ya utata wa maiti ya Sophie ambapo kwa mujibu wa baba mkubwa wake, John Kuyola, yapo mambo mengi ambayo yaliwapa shaka kutokana na kifo cha mtoto wao huyo.
Alisema kuwa, baada ya Sophie kugundulika kuwa amefariki dunia kuna mtu aliyejitokeza akajitambulisha kama baba wa marehemu na kuanza kushughulikia masuala yote lakini baadaye ilibainika kuwa ni baba wa rafiki kipenzi wa marehemu.
Alisema kuwa, ishu nyingine ni kwamba kuna polisi naye alikwenda kutoa fedha kwa ajili ya maiti kuhifadhiwa, jambo ambalo liliwashangaza wanafamilia na kuhoji ni nani ambapo alidai kuwa, yeye alitoa kwa sababu Sophie alikuwa ni mteja kwenye baa yake.
UTATA ZAIDI
Baba huyo aliendelea kusema kuwa, ndugu wa marehemu waliambiwa kwamba Sophie alifariki dunia kwa kukosa pumzi, jambo ambalo hawakukubaliana nalo hivyo kuamua kupeleka vipimo kwa mkemia mkuu ili kujiridhisha.
WANAOSHIKILIWA NA POLISI
Taarifa zinadai kwamba, hadi sasa wanashikiliwa watu watatu akiwemo Haule, aliyejifanya baba na rafiki kipenzi wa marehemu.
Mwili wa Sophia uliagwa Ijumaa iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kusafirishwa kwenda kijijini kwao wilayani Bunda, Mara kwa mazishi yaliofanyika Mei 6, mwaka huu. Marehemu ameacha mtoto mmoja mwenye umri wa miaka miwili.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, ACP Gilles Muroto alilithibitishia gazeti hili kushikiliwa kwa watu hao na kwamba uchunguzi unaendelea.
Credits: Waandishi: Issa Mnally, Richard Bukos na Gabriel Ng’osha.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com