Wajumbe wa Mtaa wapigana makonde Ofisini

WAJUMBE wawili wa Serikali ya Mtaa wa Mbondole wamezuiwa kwa siku 90 kujihusisha na shughuli za kiofisi kwa kosa la kupigana ngumi ofisini.

Imedaiwa kuwa wajumbe hao walifikia hatua kupigana mbele ya Mwenyekiti wao, Thomas Nyanduli, baada ya mmoja wao kumdhulumu mwenzake posho ya kushuhudia mauzo ya kiwanja.

Uamuzi huo wa kusimamishwa kazi wajumbe hao ulifikiwa baada ya Kamati ya Siasa ya CCM iliyoshirikisha matawi manne kuwaita na wao kukiri.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa Matawi hayo, Said Dikwembe, alisema hayo baada ya kumalizika kwa kikao hicho mwishoni mwa wiki.

Alisema baada ya kupokea taarifa ya wajumbe hao kupigana mbele ya Mwenyekiti  wa Mtaa, aliitisha kikao cha Kamati ya Siasa ya Chama ili kujadili tukio hilo.

“Tumejadili na kuwaita wajumbe hao ili kutoa utetezi wao mbele ya  wajumbe wa Kamati ya Siasa wakakiri kutenda kosa hilo, hivyo kuwapa onyo,” alisema.

Alisema pamoja na wajumbe kukiri kosa hilo, wajumbe wa Kamati waliwasimamisha kwa siku hizo 90 ili kutoa fundisho wa watumishi wengine wenye tabia kama hiyo.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mrisho Jogoo alisema tukio hilo linaonesha picha mbaya kwa wananchi, iwapo itathibitika kuwa walidhulumiana.

Alisema hilo ni jambo la ajabu kufanyika katika ofisi ya Serikali ya Mtaa mbele ya Mwenyekiti wao, kati ya Rehema Bakari na Charles Mayai.

“Unajua sielewi kwa nini suala hilo halikufika Polisi, kwani haiwezekani mwanamke kupigana na mwanamume, huo ni udhalilishaji wa kijinsia,” alisema.

Mmoja wa wajumbe hao, Mayai alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Siasa, hivyo hawezi kuzungumza lolote.

“Sina cha kuzungumza nakubaliana na uamuzi uliofikiwa na Kamati,” alisema.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com