Wabunge wawili Wagongwa na bodaboda wakitoka Bungeni Dodoma


WABUNGE wawili wamenusurika kifo baada ya kuparamiwa na kujeruhiwa na mwendesha pikipiki walipokuwa wakivuka barabara wakitokea bungeni mjini hapa jana.

Mmoja kati ya wabunge hao amelazimika kuwahishwa kwa ndege katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Wabunge waliokumbwa na ajali hiyo ni Aida Khenani, Viti Maalum (Chadema) na Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamis (CCM).

Kamanda wa Polisi mkoani humu, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, lakini alidai alikuwa bado hajapata taarifa ya kimaandishi kuhusu tukio hilo.

“Ni kweli nimepewa taarifa ya ajali hiyo, lakini siwezi kuzungumza maana bado sijaletewa kimaandishi, naomba nikupe taarifa kesho (leo),” alisema Kamanda Mambosasa baada ya kupigiwa simu na Nipashe.

Alipotafutwa na Nipashe kwa simu jana jioni, Sadifa alisema ajali hiyo ilitokea saa 5:00 asubuhi baada ya kumalizika kwa kipindi cha Maswali na Majibu bungeni.

Alisema walipata ajali wakati wabunge wakitoka nje ya viwanja vya Bunge baada ya shughuli za Bunge kusitishwa hadi leo saa 3:00 asubuhi.

“Wakati tukiwa nje ya geti tukitaka kuvuka barabara iendayo Dar es Salaam, trafiki alisimamisha magari ili tupite na magari yalisimama wabunge na wananchi wa kawaida wakaanza kupita,” alisema.

Hata hivyo, alisema wakati wakipita barabarani, mwendesha pikipiki hakusimama kama wenzake, hali iliyosababisha agonge gari lililokuwa limesimama na kushindwa kuihimili pikipiki yake na kuwaparamia watunga sheria hao.

“Bodaboda alikuwa anatufuata kutuvaa, mimi niliruka juu kuivuka pikipiki yenyewe. Sasa huyu mwenzangu (Aida), kwa sababu alikuwa nyuma, mwendesha bodaboda akamvaa,” alisema.

Sadifa alisema amepata majeraha kidogo mguuni, lakini mbunge mwenzake aliumia zaidi kichwani, mdomoni, mikono na miguu.

“Ameumia sana kichwani, hali yake ni nzuri, lakini amesafirishwa kupelekwa kwenye matibabu zaidi Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ndege ambayo imekodiwa na Ofisi ya Bunge,” alisema Sadifa.

Alisema kuwa kabla ya kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, aliwekwa katika Kituo cha Afya cha Bunge kwa mapumziko na Nipashe ilishuhudia wabunge mbalimbali wakiingia kwenye kituo hicho kumjulia hali.

chanzo Nipashe


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com