Rais aagiza Mume atakayepiga mkewe naye Apigwe


Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia wanawake wanachama wa chama tawala cha RPF-Inkotanyi (Picha/Ikulu)
Rais wa Rwanda Paul Kagame amewataka Wanyarwanda waondokane na kasumba ya kuwapiga wake zao, ambapo amesisitiza umuhimu wa kumpa kichapo mwanaume anayempiga mkewe.
Akihutubia umati wa wanawake wanachama wa RPF-Inkotanyi, wikiendi hii, Rais wa Rwanda amesema unyanyasaji wa wanawake haufai na wanaume wanaouendekeza hawana budi kupigwa ili wasirudie.
“Kwa nini awepo mtu wa kuvumilia unyanyasaji? Unyanyasaji hauvumiliki, mwanamke ndiye amefanya kazi zote za nyumbani wewe umeshinda baa, halafu ukirudi usiku unampiga?” Rais Kagame amehoji.
“Wanaume wanaowapiga wake zao ndio wanatakiwa wapigwe,” Rais Kagame ameongeza, ambapo amesema kasumba hiyo inatokana na ushauri ambao msichana anapewa na wanawake kabla ya kuolewa.
Ameukosoa utamaduni huo ambapo mwanamke mtarajiwa hufundishwa kuvumilia uonevu wa mumewe, akiambiwa kujikaza kisabuni ndiyo siri ya mwanamke kudumu kwenye ndoa.
“Msichana anaambiwa anakokwenda (kuolewa) atakutana na migogoro, kwa nini umrithishe matatizo? Eti wanaume wanapenda kuwaonea wake zao ikikutokea vumilia!” amesema Rais.
“Tunataka kukomesha unyanyasaji unaofanywa dhidi ya wanawake halafu wewe nyuma ya pazia unamuambia mtoto akipigwa asilalamike?” Rais Kagame ameongeza.
Rais wa Rwanda amesema ikitokea mwanamke apigwe, anatakiwa awaite wanafamilia wampe kipigo muonevu, ikishindikana sheria ndipo ifuate mkondo wake.
Katika hatua nyingine Rais Kagame amewakemea wanawake walioichukulia vibaya sera ya usawa wa jinsia, ambapo wapo wanaohisi inawapa haki ya kuwadharau waume zao.

Mke wa Rais Kagame, Jeannette Kagame (mbele kushoto) akiwa na Oda Gasinzigwa ambaye ni kada wa chama cha RPF-inkotanyi.

Biashara ya binadamu
Rais Kagame amesema chama chake cha RPF Inkotanyi hakitavaalia miwani suala la biashara ya binadamu, ambapo Wanyarwanda husafirishwa kwenda kuuzwa katika nchi za nje.
“Naamini mnakumbuka makumi ya wasichana waliorudishwa kutoka Uchina ambako walikuwa wamefikishwa kwa ahadi hewa za maisha bora, walikuwa kama mateka,” Rais Kagame amekumbushia.

Baadhi ya wanawake wakitabasamu wakati Rais Kagame akiwahutubia

Rais Kagame amewataka wadau wa maendeleo nchini Rwanda walivalie njuga tatizo hili, na kuwataka wasichana wajihadhari na matapeli wanaowarubuni na kisha kuyaingiza maisha yao hatarini.
Aidha Rais Kagame amewataka wazazi wawape malezi mazuri mabinti zao wanafunzi wa sekondari ambao wamekuwa wakivuka mipaka ya nchi kwenda kufanya biashara ya ukahaba nje ya Rwanda.
Rwanda ndiyo nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na wanawake wengi bungeni ambapo wamefikia asilimia 64 ya wabunge wote.

Wanawake wakicheza muziki baada ya hotuba ya Rais

Bonyeza hapa kwa picha zaidi


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com