Mmiliki wa Jamii Forum, Mwenzake Wakana Mashtaka Yanayowakabili

Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo (40), na mmoja wa wanahisa wa Mtandao wa Jamii Forum, Mike Mushi, wamekana mashtaka ya kuzuia jeshi la polisi kufanya uchunguzi yanayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mohammed Salum amedai leo mbele ya Hakimu Thomas Simba, kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo yao ya awali.
Alidai kuwa washtakiwa walizuia jeshi hilo kufanya uchunguzi kinyume na kifungu namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015.
Salum alidai kuwa kati ya Aprili Mosi, mwaka jana na Desemba 13, mwaka jana maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, washtakiwa wakiwa wamiliki wa Kampuni ya Jamii Media inayoendesha tovuti ya Jamii Forum, walishindwa kutoa taarifa kuhusu mmiliki wake huku wakijua kwamba jeshi hilo linafanya uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyochapishwa kielektroniki kwenye tovuti hiyo.
Alidai kuwa washtakiwa wanamiliki kampuni hiyo iliyosajiliwa kisheria na kwamba wanacheti cha kuendesha biashara ya mtandao.
Pia alidai taratibu za kujiunga katika mtandao huo mtu anatakiwa kujisajili hivyo wakiwa kama wahusika wa kampuni hiyo wanajua watu wote na shughuli wanazozifanya.
Salum alidai Kamanda wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alimuandikia barua mkurugenzi wa kampuni hiyo kuhusu taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao huo.
Aliendelea kudai kuwa kamanda huyo alitaka apewe taarifa za mtu binafsi kuhusu taarifa zilizochapishwa ili aisaidie polisi kufanya uchunguzi na kwamba washitakiwa hao walikataa kwa sababu zao.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa walikana maelezo yote isipokuwa umri, majina, makazi na kazi zao.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 2 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Hata hivyo, kesi hiyo ilitajwa tena mbele ya Hakimu Victoria Nongwa ambapo upande wa mashitaka uliowakilishwa na Wakili Salum, ulidai utaleta mashahidi saba  kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma hizo. Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 3 mwaka huu.
Na Denis Mtima/GPL


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com