Mfanyabiashara achomwa visu 14 na kaka yake

Mfanyabiashara wa samaki, Warioba Mtatiro, mkazi wa Kijiji cha Etalo, Musoma Vijijini, mkoani Mara nchini Tanzania amedaiwa kujeruhiwa vibaya kwa kisu na kaka yake.
Tukio hilo la limetokea hivi karibuni katika Mtaa wa Nyamulinda, Kijiji cha Etalo, Musoma Vijijini kwa mujibu wa Global Publishers ambao ndio chanzo cha habari hii.
Kwa mujibu wa chanzo kilichoshuhudia mtiti huo, Mtatiro alikuwa akicheza kamari maarufu mkoani Mara kwa jina la Magaramka na kaka yake ndiye aliyekuwa akichezesha.
Alisema baada ya ‘kupunwa’, Mtatiro hakuwa na kiasi hicho cha fedha kilichohitajika katika mchezo huo ndipo ugomvi ukaibuka hadi kufikia hatua ya kaka kumchoma visu mdogo wake.
“Mtatiro alipunwa shilingi mia tano. Sasa kaka yake akawa anamdai na yeye akawa hana ndipo alipoamua kuchukua kisu na kuanza kumchoma.”
“Alimchoma sehemu mbalimbali mwilini, kichwani na mgongoni na kumsababishia majeraha makubwa. Kwani alikuwa anachoma kisha anachomoa na kuchoma sehemu nyingine kama mara 14,” kilisema chanzo hicho.
Hivi ndivyo alivyo hospitalini baada ya kucomwa visu
Chanzo hicho kilieleza kuwa, baada ya watu kuamulia, kaka mtu alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Musoma kwa ajili ya hatua za kisheria huku majeruhi akikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Majeruhi huyo anafanya biashara ya kuuza samaki katika kontena la samaki lililopo Mtaa wa Nyamulinda, jirani na eneo walilokuwa wakicheza kamari hiyo.
Akizungumza na Risasi Jumamosi kwa shidashida mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, Mtatiro alisema kaka yake huyo alimchoma visu hivyo baada ya kushindwa kumlipa shilingi 500 aliyomshinda kwenye kamari.
“Baada ya kunipuna nilimwambia sina lakini yeye hakutaka kunielewa, akaanza kunishambulia kwa visu.
Kanichoma sana visu mgongoni, nashukuru Mungu kama si watu kuniamulia, angeniua
yule,” alisema Mtatiro.

Risasi Jumamosi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Jafari Mohamed kuhusiana na tukio hilo ambapo alipopatikana alisema bado halijamfikia.

“Nashukuru kwa kunipa hizo taarifa, nitazifanyia kazi maana bado hazijafika mezani wangu hivyo nitafuatilia,” alisema Kamanda Mohamed.
Chanzo:Gazeti la Risasi


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com