Kauli ya Mkwasa Kuhusu Yanga Kufulia


Katibu mkuu wa klabu ya Yanga Bw. Charles Boniface Mkwasa amekanusha kwamba klabu hiyo ina hali mbaya kiuchumi na kufikia kuomba msaada wa kuchangiwa na wanachama wake.

Mkwasa amesema, Yanga imefungua account maalum kwa sababu kwa muda mrefu wanachama wamekuwa wakiomba kuichangia klabu yao kwa chochote walichonacho. Mkwasa ambaye amewahi kuitumikia Yanga akiwa mchezaji na baadae kocha kabla ya sasa kuwa katibu amesema Yanga bado ipo imara ndio maana timu inasafiri, inashinda mechi zake bila ya kuwa na madeni ukiachana na yale ya zamani ambayo wanapambana kuyalipa.

“Tunaposema kwamba hatuna fedha si kama hatuna fedha kwa kiasi ambacho wanafikiria watu wengine, Yanga ni brand kubwa na ina wigo mkubwa wa kupata mapato. Kuna wanachama mbalimbali wanajitolea bila kutaka majina yao kutangazwa kwenye vyombo vya habari, kuna mapato ya getini .”

“Hili suala limechukuliwa tofauti na baadhi ya wapinzani wetu wengine wakisema kwamba sisi hatuko vizuri kiuchumi kitu ambacho si kweli, timu imekuwa ikicheza, ikisafiri na kushinda ,mechi zake kwa kipindi na hakuna sehemu ambayo tumeacha deni ukiachilia mbali madeni ya zamani ambayo tumekuwa tukiyapunguza na ndio maana tumehitaji mchango wa wanachama kwa sababu ndio wenye timu.”

“Tatizo la kudaiwa mishahara na wachezaji wetu sio sisi tu, hata makampuni makubwa yanadaiwa mishahara na wafanyakazi hadi mengine kufikia uamuzi wa kupunguza wachezaji. Kuna timu zingine zinaogopa kutanga kudaiwa mishahara na wachezaji kwa sababu wanahofia kuonekana tofauti.”

“Yanga bado ipo imara na inaweza kuendelea na shughuli zake tofauti isipokuwa pale ambapo tunahitaji kupata msaada kutoka kwa wanachama basi ina fursa ya kuwatumia wanachama wake kuweza kuchangisha kile wanachoweza kuchangia.”

Hivi karibuni, inadaiwa wachezaji wa Yanga walitaka kugoma kucheza mchezo wa kimataifa wa kombe la shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger kutokana na kutolipwa mishahara yao kwa muda mrefu. Hata hivyo siku chache baada ya mchezo huo  uliochezwa hapa Tanzania, mshambuliaji wa klabu hiyo Obrey Chirwa aligoma kusafiri kwenda Algeria kucheza mechi ya marudiano akishinikiza alipwe mishahara yake anayodai.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com