Daktari afikishwa kortini akituhumiwa kula rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Shinyanga imewafikisha mahakamani watumishi watatu wa hospitali binafsi ya Kolandoto, akiwamo Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Elimeleki Katani, kwa tuhuma za rushwa.


Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, ilieleza kuwa washtakiwa wengine waliofikishwa katika mahakama hiyo ni Mhasibu Mkuu, Samson Challo na Mhasibu Msaidizi Hamis Batano, wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya ruzuku ya serikali.

Washtakiwa hao walifikishwa kwenye mahakama hiyo mwanzoni mwa wiki hii mbele ya hakimu mfawidhi, Rahimu Mushi, na kusomewa mashtaka yao yanayowakabili na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Carsorn Nkya.

Katika shtaka la kwanza upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa kati ya Juni 10, mwaka 2011 na Januari 1 mwaka 2016 washtakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kurejesha kwa mlipaji mkuu wa serikali mshahara wa mstaafu Dk. Emmanuel Mwandu Sh. 63,479,800.

Kwenye shtaka la pili upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa kati ya Septemba 18 mwaka 2013 na Agosti 21 mwaka 2014 washtakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kuandaa na kupeleka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) michango ya mstaafu Dk. Emmanuel Mwandu Sh. 14,361,124.

Katika shtaka la tatu upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa kati ya Mei 30 mwaka 2011 na Januari 6 mwaka 2014, Hamis Batano alitumia madaraka yake vibaya kwa kuandaa orodha ya malipo kama mshahara wa wastaafu Dk. Emmanuel Mwandu kiasi cha Sh. 14,361,124.

Katika shtaka la nne upande wa mashataka uliiambia mahakama kuwa kati ya Juni 10, mwaka 2011 na Januari 1 mwaka 2016 washtakiwa kwa pamoja waliisababishia serikali hasara kutokana na malipo hewa ya mstaafu Dk. Emmanuel Mwandu.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka yao walikana na kupatiwa dhamana baada ya kutimiza masharti.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 13, mwaka huu kwa ajili ya usikilizaji wa hoja za awali na washtakiwa wako nje kwa dhamana.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com