Ambao Hamjawapeleka wanafunzi shule Mpaka sasa Mtakoma - DC Sanga


Na Mwamvua Mwinyi, Mkuranga

MKUU wa wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Filberto Sanga amewataka wazazi ambao watoto wao wamefaulu kuingia kidato cha kwanza kuwapeleka shule mara moja, na atakaebainika kukaa na mtoto nyumbani atakiona. 

Aidha amewataka wazazi wenye
watoto waliofikia umri wa kuanza darasa la kwanza kwenda kuwaandikisha bila kufanya ajizi. 

Amesema kuanzia sasa ataambatana na timu yake, kupita kuhakiki kijiji hadi kijiji na endapo atakutwa mtoto hajapelekwa shule mzazi wake atafikishwa mahakamani. 

Sanga alisema msimamo huo,wakati akizungumza katika kata ya Msonga, Magawa, Njianne, Kitomondo na Mwarusembe wilayani hapo kwenye mikutano ya ndani iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani. 

Alieleza licha ya serikali kuagiza elimu kutolewa bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne lakini wapo wazazi mpaka sasa wanaoshindwa kuwapeleka shule watoto wao kwa sababu zisizoeleweka.

Sanga alisema atalivalia njuga suala hilo hadi hapo atakapohakikisha watoto hao wameripoti mashuleni. 

Alifafanua kwamba sekta ya elimu haina utani hata kidogo na ni haki ya mtoto .

Sanga alibainisha kwamba, watoto bila kuwa na elimu wilaya hata mkoa na taifa haitojikomboa.

"Asilimia 80 ndio walioripoti mashuleni wengine wapo majumbani ,hivyo wazazi wawe na mwamko wa elimu ili kuwakomboa watoto wao”

“Serikali inachangia vitu vyote vya msingi ,sioni sababu ya mzazi kukaa na bila elimu, atakaekaidi agizo hili afikishwe mahakamani”alisisitiza Sanga. 

Kwa upande wake,katibu wa siasa na uenezi CCM mkoani Pwani, Zainab Gama, aliwataka wazazi kuwalinda na kuwalea watoto kwa umoja kwani mtoto wa mwenzio ni wako. 

Alisema vijana wengi wanaharibika kutokana na kuiga maadili ya nchi za nje na kushawishiana. 

Gama aliiomba jamii kukemea watoto na vijana ambao wanakiuka mila, desturi na maadili ya nchi bila kuwaonea aibu. 

Nae katibu wa CCM wilaya ya Mkuranga, Abihudi Shilla alisema anaunga mkono suala la watoto kufikishwa shule kwa wakati kwa kuwa anatambua umuhimu wa elimu.

Shilla anasema, endapo watu wanachangia harusi na sherehe kuna kila sababu ya kuipa kipao mbele elimu ili kuwajengea watoto msingi bora katika maisha yao ya baadae. 


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com