Wanafunzi wasomea Barazani baada ya Kukosa Darasa

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kingo iliyopo kijiji cha Kwamba kilichopo kata ya Songe wilayani Kilindi,wanalazimika kusomea nje kwenye baraza kwa sababu ya upungufu wa vyumba vya madarasa hatua ambayo wakati wa mvua wanafunzi wa madarasa mawili hulazimika kuingia chumba kimoja kisha kufundishwa kwa zamu.

Kwa mujibu wa kituo cha ITV kimeshuhudia wanafunzi hao wakiwa wamekaa kwenye madawati nje ya chumba cha darasa huku mwalimu wao ambaye ni makamu mkuu wa shule hiyo Aziz Simba akibainisha kuwa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa ni kubwa na wameiomba serikali na wasamaria wema kusaidia tatizo hilo.

Mwakilishi wa wazazi wa shule ya msingi Kingo Ngulelo Ole Matagi amesema wanashukuru serikali kuwapatia walimu lakini wameomba waongezewe nguvu kwa sababu jitihada za wazazi za uchangiaji wa fedha hadi kufanikisha ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa ambapo kati ya hivyo vitatu wanavyosomea wanafunzi ndio ambavyo vimekamilika zimeanza kupungua.

Jitihada za kumpata Afisa Elimu ya msingi wilayani Kilindi Geofrey Abayo kuelezea hatua hiyo bado zinaendelea baada ya kuelezwa kuwa yupo nje ya wilaya kikazi.

Andika maoni yako hapa (MATUSI HAPANA) 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com