Taarifa ya Msiba kutoka Yanga Sports Club

yanga
Uongozi wa klabu ya soka ya Yanga unasikitika kutangaza kifo cha mwanachama wake Mhe Hafidh Ally Tahir kilichotokea mjini Dodoma tarehe 10/11/2016.
Mhe Hafidh Ally Tahir – ambae Pia alikuwa mbunge wa CCM Jimbo la Segerea Dimani Zanzibar amefariki akiwa anapitiwa matibabu katika hospital ya General mkoani Dodoma.
Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir alikuwa ni miongoni mwa Marefa wa mwanzo wa FIFA barani Afrika ambapo amechezesha mechi za soka za kimataifa.

Katika maisha yake, Mheshimiwa Hafidh Ally pia alikuwa mtangazaji wa iliyokuwa Redio Tanzania ambapo miongoni mwa manguli aliyofanya nayo kazi ni Marehemu David Wakati “Magunia”.
Katika utawala wa Rais wa Tano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ); Mheshimiwa Hafidh Ally alikuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Aidha Mheshimiwa Hafidh Ally ashawahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Rahaleo.
Mheshimiwa Hafidh Ally alikuwa ni mwanasoka hadi dakika ya mwisho kwani alichezea timu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Yanga iliyoinyuka ile timu shindani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Simba, ambapo alifunga magoli matatu katika mechi hiyo.
Siku moja kabla ya mauti kumfika Mheshimiwa Hafidh Ally alichaguliwa kuwa Katibu wa Timu hiyo ya Bunge, chini ya Uenyekiti wa Mbunge wa Kilolo Mheshimiwa Mwamoto.
Mchango wake Mkubwa utakumbukwa daima na sote tunaungana na familia yake, wananchi wa jimbo la Dimani chini ya Mwakilishi Mheshimiwa MwinyiHaji Makame Mwadini, Wazanzibari wote chini ya Kiongozi wetu Dkt Ali Mohamed Shein – Rais Wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia Watanzania wote chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli.
Yanga inatuma salamu za rambirambi maalum kwa Waheshimiwa Wabunge wote na Watumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi Mahiri wa Mheshimiwa Job Ndugai (Mb) – Spika wa Bunge.
Uongozi was Yanga utashiriki kikamilifu katika mazishi huko visiwani Zanzibar.

Imetolewa na Uongozi,

Young Africans Sports Club!


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com