Kasi ya Maambukizi ya VVU Yamuacha Hoi Mkuu wa WilayaAmtaka mganga mkuu na waatalamu wa afya kutoa elimu kwa wananchi wa Kamsamba juu ya maambukizi ya ukimwi.
;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;;

Mkuu wa wilaya ya Momba, Mhe. Juma Said Irando ameshtushwa na kasi kubwa ya maambukizi ya ukimwi katika tarafa ya Kamsamba wilayani Momba.

Masikitiko hayo aliyaonyesha alipotembelea Kituo cha afya cha Kamsamba.

Akihojiwa na Mkuu wa wilaya,Kaimu mganga mfawidhi wa kituo hicho Stanley Simbeye alimueleza mkuu wa wilaya kuwa kituo chake kinahudumia wastani wa wagonjwa 60 kwa siku, wagonjwa wengi wakigundulika kusumbuliwa zaidi na magonjwa ya Malaria, matatizo ya tumbo, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) na kwa kiasi kikubwa maakumbikizi ya Ukimwi na magonjwa ya Zinaa.

Akimjibu Mkuu wa wilaya alipotaka kujuwa hali ya maambukizi ya ukimwi katika kituo chake, Kaimu mganga mkuu alimueleza mkuu wa wilaya kuwa kasi ya maambukizi ya ukimwi ipo juu katika kata ya Kamsamba na vijiji vya jirani.

 akifanunua zaidi Dk.Simbeye alisema kuwa kati ya wagonjwa kumi wanaopimwa maambukizi ya ukimwi sita hugunduliwa kuwa na maambukizi sawa na asilimia 60, hali iliyomtisha mkuu wa wilaya na kumuagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Momba kupelekea wataalamu wake wa afya kukutana na wananchi wa vijiji hivyo na kutoa elimu ya kukabiliana na kasi hiyo ya maambukizi kwa wananchi hao.

Akizungumza na kamati ya maendeleo ya kata hiyo ya Kamsamba Irando alitaka kujua sababu za ongezeko la kasi ya maambukizi na mikakati yao katika ujenzi wa uzio wa kituo hicho cha afya, kamati hiyo ilimueleza Mkuu wa wilaya kuwa sababu kubwa ya ongezeko la maambukizi ya ukimwi katika kata hiyo ni kutokana na mwingiliano mkubwa wa wafanyabiashara wa mpunga wanaotoka sehemu mbalimbali, wavuvi wa samaki wanaovua katika ziwa rukwa, ulevi,ndoa za utotoni na ukosefu wa elimu afya juu ya maambukizi ya ukimwi.

Kuhusu kukabiliana na tatizo la ukosefu wa uzio wa kituo hicho cha afya, madarasa na nyumba za watumishi, kamati hiyo hiyo ilimueleza Dc Irando kuwa wamekubaliana na wananchi wa kata hiyo kutengeneza  jumla ya matofali 360,000 kwa awamu tatu hivyo yatakapokuwa tayari wataomba nguvu ya Serikali kukamilisha ujenzi wake, Dc Irando aliitaka kamati hiyo kuanza na ujenzi wa uzio wa kituo hicho cha afya mapema kutokana na umuhimu wake kiusalama kwa wagonjwa wanaofika katika kituo hicho kupata huduma na hata usalama wa watumishi na wauguzi wa kituo hicho.

Akiongelea suala la nishati ya umeme katika kituo hicho Dc Irando aliiambia kamati hiyo ya maendeleo kuwa umeme tayari umeshafika katika kituo hicho na utawashwa katikati ya mwezi huu.

Naye afisa Mtendaji wa kata ya Kamsamba alimueleza mkuu wa wilaya kuwa kata yake inaundwa na jumla ya vijiji 6 venye kaya 3644 zenye wakazi 18210 na changamoto kubwa wanayokabiliana nayo katika kata yake ni tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa ambapo wananchi wa vijiji hivyo hulazimika kufata maji ziwani au katika mto Momba ambapo hulazimika kutembea umbali wa takribani kilometa 10 hadi 15 kufata huduma hiyo.

Irando pia alikagua ujenzi wa jengo la upasuaji linalojengwa katika kituo hicho cha afya kwa ufadhili wa Shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) pamoja na kutembelea wodi za wagonjwa.
Akihitimisha ziara yake kituoni hapo mkuu wa wilaya alifanya kikao na wauguzi na watumishi wa kituo hicho, ambapo aliwapongeza kwa huduma ya kuridhisha wanayotoa, pia aliwapongeza kwa juhudi zao za kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya wa jamii (CHF) na kuwataka kuendelea kuhamasisha utoaji wa elimu juu ya umuhimu wa wananchi kujiunga na mfuko huo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Momba aliyeongozana na Mkuu wa wilaya Adrian Jungu aliwaambia wauguzi na watumishi wa hospitali kuwa Serikali inafahamu juu ya upungufu wa watumishi na wauguzi katika kituo hicho na anajitahidi atakapopata watumishi atawaongeza ili kukabiliana na changamoto na kuwashukuru kwa moyo wao wa kizalendo na kuwapongeza kwa juhudi zao za kufanya kituo hicho kujiendesha chenyewe bila utegemezi wa Serikali kwa kutunisha mfuko wao wa afya ya jamii na kutokuwepo kwa tatizo la upungufu wa madawa katika kituo hicho.


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com