Hivi Ndivyo Rais Magufuli alivyoongoza Wananchi Kumuaga Marehemu Joseph Mungai

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Mzee Joseph Mungai, aliewahi kuwa Waziri katika Wizara mbalimbali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuanzia Awamu ya kwanza mpaka ya nne, ulioagwa leo katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es salaam.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimpa pole mjane wa Marehemu Mzee Joseph Mungai.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 10 Novemba, 2016 amewaongoza viongozi na wananchi wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa Waziri na mbunge Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph James Mungai katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam. 

Pamoja na Rais Magufuli Viongozi wengine waliofika kuuaga mwili wa Marehemu Mungai ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Makamu wa Rais Mstaafu Mhe. Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Frederick Tluway Sumaye, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Viongozi wengine mbalimbali wa Serikali na Siasa.

Mhe. Joseph James Mungai alifariki dunia tarehe 08 Novemba, 2016 katika hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua ghafla na mwili wake utasafirishwa kesho Ijumaa kwenda Mafinga Mkoani Iringa kwa Mazishi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewatembelea na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Sewahaji iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam wakiwemo Waziri na Balozi Mstaafu wa Tanzania Mhe. Omar Ramadhan Mapuri na Mkewe Mama Janeth Magufuli.

Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo wamemshukuru Rais Magufuli kwa hatua zilizochukuliwa na Serikali kuboresha hospitali ya Taifa Muhimbili na wamebainisha kuwa licha ya kuboreshwa kwa mazingira ya hospitali pia wanapata huduma nzuri kutoka kwa madaktari na wauguzi.

Mapema leo asubuhi, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mfadhili wa Taasisi ya Gatsby Tanzania Lord Sir David Sansburg na kumuhakikishia kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza kilimo, wajasiriamali na viwanda ambazo zinafanywa na Taasisi hiyo.

Dkt. Magufuli amesema atafurahi kuona Taasisi hiyo ambayo imekuwa ikiwasaidia wakulima wa pamba na chai kupata mbegu bora na kusindika mazao yao, inapiga hatua zaidi kwa kuanzisha viwanda vya nguo na kwamba Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Novemba, 2016


JIUNGE NA eddy blog SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Eddy Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com