NEC: Sasa waliopoteza Vitambulisho Kupiga Kura


NEC-DODOMA 


Tume ya Taifa ya uchaguzi imesema kuwa Wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Madiwani wa Kata 43 unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu. 

Hayo yamesemwa leo (16.10.2017) na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Ramadhani Kailima Mjini Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasiadizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa na NEC. 

Bw. Kailima amesema wapiga kura hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Hati ya kusafiria na Leseni ya udereva. 

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambacho kinasema mpiga kura aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda mwenyewe kwenye Kata aliyojiandikisha na kituo alichopangiwa” Amesema. 

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni kumridhisha msimamizi wa kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye ndiye mpiga kura halali na kuongeza kuwa kifungu hicho kinamtaka Mpiga Kura aonyeshe kadi yake ya kupigia. Aidha, kinaeleza kwamba Tume inaweza ikaelekeza utambulisho mwingine wowote utakao msaidia mpiga kura kuweza kupiga kura iwapo hana kadi. 

Bw.Kailima amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu hicho, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26, 2017 imetoa maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi kuruhusu wapiga Kura waliojiandikisha kwenye Dafatari la kudumu la Wapiga Kura kutumia Hati ya kusafiria, kitambulisho cha Taifa kilichotolewa na NIDA na leseni ya udereva. 

Bw. Kailima amesema ruhusa hiyo imetolewa kwa sharti moja kwamba majina na herifu yaliyopo kwenye kitambulisho hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. 

Ameongeza kuwa NEC itakutana na vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu ya maagizo hayo na kusisitiza kwamba tofauti yoyote itakayo kuwepo kwenye majina itamnyima mpiga kura fursa ya kupiga kura. 

Bw. Kailima amesema maamuzi hayo yamefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa mwaka 2015. 

“ Katika kipindi chote hichi (2015-2017) inawezekana kwa namna moja ama nyingine, kuna baadhi ya wapiga kura wamepoteza kadi zao za kupigia kura na kwa sababu hatujaboresha na sheria inasema watapata hizo kadi baada ya daftari kuboreshwa, wanaweza wakakosa fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa madiwani wa kata 43, lakini wengine kadi zao zimeharibika kiasi kwamba haziwezi kusomeka, na wengine kadi zao zimechakaa kabisa kwa sababu moja ama nyingine kutokana na mazingira yaliyopo,” amesema. 

Wakitoa maoni yao juu ya agizo hilo la NEC, washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza hatua hiyo na kusema kwamba itakuza wigo wa demokrasia nchini kwa kuwapa fursa wapiga kura halali ambao kwa sababu zilizoko nje ya uwezo wao wamejikuta hawana kadi za kupigia kura licha ya kwamba ni wapiga kura halali waliojiandikisha. 

Bw. Abdul Kasembe ambaye ni Afisa Uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma amesema kuwa amefurahishwa na uamuzi huo akieleza mambo mengi yamejitokeza kati ya mwaka 2015 mpaka sasa. 

“Sisi tumefurahia agizo hili kwa kuwa litawapa fursa wananchi ambao pengine wangeikosa fursa kwa kuwa hawana kadi japokuwa wamejiandikisha”. 

Bi. Margaret Nakayinga, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Mkoani Tabora amesema agizo hilo limeleta fursa kwa watu ambao pengine wangekosa fursa ya kupiga kura kwa kupoteza kadi ya kupigia kura au kwa kuharibika kwa kadi zao. Tutakaporudi huko tutawatangazia wananchi ili wajitokeze kwa wingi kupiga kura..”. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mkoani Tanga, Bw. Kazimbaya Makwega amesema kuwa agizo hilo ni muafaka na limezingatia mazingira ya Kitanzania kwa kuwa watu wanaweza kupoteza kadi au kuharibikiwa na kadi zao na kukosa fursa ya kupiga kura.


Angalia Madini ya Makaa ya Mawe yalivyotapakaa ardhini Mchuchuma Ludewa

Waandishi wa habari kutoka Njombe Press Club wametembelea eneo la Mchuchuma lililopo wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe na kujionea hazina kubwa ya makaa ya mawe yaliyogundulika wilayani humo

Aidha imebainika kuwa madini hayo yapo kwa wingi katika wilaya hiyo na uchimbaji wake unatarajiwa kulinufaisha taifa kwa kuingiza kipato cha serikali pamoja na wananchi 

Angalia Picha hizi:-

 Waandishi hao wakiwa wameshika Makaa ya mawe Yalipo sehemu tu ya Makaa ya mawe yanayoonekana juu ya ardhi
 Wanahabari wakiendelea kuyaangalia makaa ya mawe
 Muonekano wa makaa ya mawe
 Wa kuyabeba na kuyashika hayaaaa....


Wagonjwa waenda na mashuka, neti zao hospitali

Hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mashuka, blanketi pamoja na vyandarua, hali ambayo inawalazimu wagonjwa kuchukua na kutumia mablanketi na mashuka kutoka majumbani mwao

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Kahama Dr. Fredrick Malunde amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na nyinginezo zinazoikabili hospitali hiyo, ambapo pia amesema hospitali imeelemewa na wagonjwa wanaolazwa kwa idadi ya 30,000 kwa mwezi, huku kukiwa na wastani wa wagonjwa 200 wanaolazwa kwa siku.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kahama mji Bi. Flora Sangiwa amesema uchakavu wa miundombinu ya matibabu katika hospitali ya Kahama, unachangiwa na ufinyu wa bajeti inayotengwa lakini pia hospitali inahudumia wagonjwa wengi kutoka nje na ndani ya wilaya hiyo.
Kufuatia hali hiyo baadhi ya wadau wa afya wilayani humo wamejitokeza na kuanza kutatua changamoto hiyo ambapo Benki ya Posta Tanzania tawi la Kahama wametoa mashuka 100 na vyandarua 50, huku wakidai kuendelea kutoa msaada zaidi kwa lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo.


Ludewa: Walimu wamwagia chumvi kwenye choo cha wanafunzi ili Kisijae

 Choo cha wavulana ambacho kimejaa lakini humwagiwa chumvi ili kupunguza ujazo wa kinyesi na choo hicho kiendelee kutumika
 Choo kipya kinachojengwa na mdau mpenda elimu kutoka Ludewa
Mdau huyo Augustino Mwinuka akiongea na wanahabari

Baada ya kuvutiwa na jitihada za aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, Mdau wa maendeleo Ludewa ameamua kujitoa kusaidia ujenzi wa vyoo shule ya msingi Ludewa Mjini ambapo wanafunzi wanatumia vyoo vilivyojaa baada ya waalimu wao kuvijaza maji na Chumvi ili kupunguza ujazo wa kinyesi katika vyoo hivyo.

Mdau huyo mkazi wa Ludewa, Mkoani Njombe, anayefahamika kwa jina la  Agustino Mwinuka  amesema licha ya Shule hiyo kuwa na changamoto ya vyoo ila juhudi alizoonyesha Mbunge wao enzi za uhai wake zimemsukuma na yeye kuchangia kwenye maendeleo ya kusaidia kuboresha mazingira ya shule hiyo. 
"Mimi nimevutiwa na jitihada zilizokuwa zimefanywa na aliyekuwa Mbunge wetu Deo Filkunjombe enzi za uhai wake. Madarasa aliyajenga vizuri sana na yapo 'standard' tatizo lipo kwenye vyoo hivyo mimi kama mdau wa maendeleo wilayani Ludewa nimeona niaze hili kuhamasisha" amesema Mwinuka 
Kwa upande wa Mwalimu Mkuu Mathew Haule wa shule hiyo amesema kuwa vyoo hivyo pamoja kuwa ni vya shimo bado haviwatoshi wanafuzi wa shule na kuongeza kuwa tayari vimejaa na shule imefanya jitihada za kuweka maji na chumvi ili kushuka chini.
"Vyoo ni tatizo katika shule yetu, kwa wavulana yanahitajika matundu 12 lakini kwa sasa yapo 10 tu na yamejaa pia. Tunahitaji msaada". Mwalimu Haule 
Licha ya kuwa na vyoo vilivyo choka vya shimo, wanafunzi wa  darasa la tano mpaka la saba wanatumia Madarasa ya kisasa yaliyojengwa na Marehemu Filikunjombe.
Deo Filikunjombe alifariki Oktoba 15, 2015 kwa ajali ya helkopta iliyoanguka kwenye msitu wa hifadhi ya Selous akitokea Dar es salaam kwenda Ludewa, akiwa na rubani wake William Silaa ambaye ni baba mzazi wa Jerry Silaa, na msaidizi wa Deo Filikunjombe, Bwana Mkwera ambao pia walifariki dunia.


Mapya haya: Kanumba kumpandisha Lulu kizimbani

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam inatarajia kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi ya mauaji bila kukusudia inayomkabili Msanii wa filamu nchini Tanzania, Elizabeth Michael maarufu kama ‘Lulu’.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya kesi za mauaji ya bila kukusudia iliyotolewa na Mahakama Kuu, kesi ya Lulu itaanza kusikilizwa siku ya Oktoba 19/2017 mbele ya Jaji Sam Rumanyika.
Lulu anakabiliwa na kesi hiyo akidaiwa kumuua Msanii mwenzake, Steven Kanumba bila kukusudia kinyume cha kifungu cha 195 cha kanuni za adhabu (PC), April 7/2012 nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican.
Lulu na Kanumba walidaiwa kuwa ni wapenzi ambao mapenzi yao yalikuwa na siri kubwa mpaka tukio la kifo lilipomkuta Kanumba ndipo ilipofahamika juu ya mahusiano yao. 


113 Wajitokeza Kuwania Uenyekiti UVCCM

Wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) 113 kutoka bara na visiwani wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti Taifa katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu, idadi ambayo haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa umoja huo.

Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Mbunge wa Donge Visiwani Zanzibar, Sadifa Juma Khamis ambaye alichaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2012.

Akizungumza jana Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Shaka Hamidu alisemma wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM linafanya usahili wagombea waliomba nafasi mbalimbali za uongozi.

Alisema usahili huo unafanyika kwa waliomba kugombea wa nafasi za mwenyekiti, makamu, wajumbe watano wa halmashauri kuu ya Taifa (NEC), wajumbe watano wa baraza kuu la umoja huo Taifa na wajumbe wa kuwakilisha jumuiya hiyo katika jumuiya nyingine za chama.

Alisema zoezi hilo ambalo limeanza tangu Aprili limefanikisha kupatikana kwa viongozi mbalimbali wa ngazi za shina hadi wilaya na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi za kitaifa.

“Vijana 113 wamejitokeza kuomba nafasi ya uenyekiti. Huu utakuwa ni uchaguzi wa kihistoria kati ya chaguzi zote zilizowahi kufanyika tangu mwaka 1978 ilipoanzishwa jumuiya hii mwaka huu. Kwa maneno mengine tumevunja rikodi,”alisema.

Alisema kwa upande wa nafasi ya umakamu mwenyekiti waliomba kugombea ni 23 wakati ujumbe wa Nec 118 wanachuana kugombea nafasi tano zilizopo kikatiba.

Shaka alisema jumla ya wagombea ambao wanawafanyiwa usahili katika kikao cha Kamati ya Utekelezaji wa baraza la Kuu la UVCCM ni 375 huku nafasi ya uenyekiti Taifa ikiongoza kwa waombaji wengi katika zoezi hilo.

Kwa mujibu wa Shaka, Kamati ya utekelezaji ni kikao cha awali ambacho kitatoa mapendekezo kwa Baraza Kuu la Taifa la umoja huu ambalo litakutana Oktoba 17 kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya kamati hiyo.

“Baraza Kuu litakutana hapa hapa Dodoma kwa ajili ya kupokea na kupendekeza nafasi zilizoombwa katika mikoa na Taifa. Sisi (Baraza Kuu la umoja huo) tunapendekeza kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,”alisema .

Kwa mujibu wa utaratibu CCM kikao kitakachowachuja wagombea wa nafasi zote ambazo zinauwakilishi wa chama taifa ni Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inayoongozwa na Mwenyekiti wake wa Taifa Dk John Magufuli.

Akizungumzia kuhusu chaguzi zilizopita za mashina hadi wilaya, Shaka alisema kuwa mambo yamekwenda vizuri katika chaguzi zote.

Alijitapa kuwa chama chao siku zote kimekuwa kikisimamia haki na usawa ili vijana waweze kupata fursa kwa nafasi wanazoziomba katika chaguzi mbalimbali nchini.

“Katika ngazi wilaya kuna changamoto mbalimbali kwenye uchaguzi ambazo zimejitokeza lakini jumuiya hii inaongozwa na kanuni na katiba ya chama chetu kwa hiyo tumeagiza viongozi wetu kuhakikisha kuwa wanashughulikia malalamiko yaliyojitokeza,”alisema

Alisema malalamiko yaliyojitokeza katika chaguzi hizo ni pamoja na hofu kuwa kuna wagombea wamezidisha umri na dhana ya kutumia rushwa.

Hata hivyo, alisema chama hicho kimekuwa kikikemea vitendo vya rushwa na hivyo itakapothibitika uvunjaji wa kanuni watachukua hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

“Hatutadharau malalamiko yoyote yake, yote yatashughulikiwa na atakeyabainika kuvunja kanuni hatua zitachukuliwa,”alisema


Nape: Kuzuiwa mikutano ya kisiasa si kuminya demokrasia

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema kuzuiwa mikutano ya kisiasa si kuminya demokrasia kwa kuwa  kuna bunge ambalo linaweza kutumika kutolea maoni yao. 

Akihojiwa na kituo cha Televisheni cha  KTN kutoka nchini Kenya katika kipindi cha siasa za kanda kuhusu demokrasia katika Afrika, Nape amesema demokrasia inatakiwa kutafsiriwa kulingana na maeneo tuliyopo.

“Afrika hatuwezi kuwa na demokrasia iliyo sawa na Marekani,” amesema.

Nape alitakiwa kutoa maoni yake kuhusu viongozi wa Chadema kudai kwamba, Rais John Magufuli anaminya demokrasia hasa kuzuia mikutano ya hadhara.

Akijibu, Nape amesema nchi za Afrika hazitakiwi kutafsiri demokrasia kwa kujilinganisha na nchi zilizoendelea za Magharibi.

“Hapa kwetu baada ya uchaguzi mkuu tunaruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yetu haturuhusiwi kufanya mikutano nje ya majimbo yetu,” amesema.

Amesema uchaguzi ukishamalizika siasa zinahamia bungeni ambako wabunge wanaweza kutoa maoni yao.

“Sioni kama hapa demokrasia inaminywa au kuna udikteta kwa sababu hiyo inawahusu wabunge wote kutoka chama tawala na vyama vya upinzani,” amesema.

Nape ambaye alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema zamani wanasiasa waliruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Nape amesema wakati wa uchaguzi mkuu shughuli nyingi huwa zinasimama kwa sababu ya mikutano ya wanasiasa.

“Kwa hiyo kuna umuhimu wa viongozi wa kisiasa kwenda kutekeleza yale waliyowaahidi wananchi,” amesema.

Nape amewataka wasomi kutoa tafsiri kwa upana kuhusu dhana ya demokrasia  ili wananchi waweze kuitekeleza kulingana na maeneo waliyopo.


Nkamia: Nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu binafsi ya ukomo wa Bunge

Mbunge  wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, ameondoa kwa muda kusudio lake la kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba ya nchi ili kuongeza ukomo wa ubunge.

Nkamia aliwasilisha kusudio hilo Septemba, mwaka huu mjini Dodoma kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016, kupitia barua yake aliyoisaini Septemba 12, mwaka huu  iliyokuwa ikipendekeza kuongeza muda wa Bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kupunguza muda wa uongozi wa vijiji kutoka miaka mitano hadi minne.

Kupitia ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, Nkamia alisema ameamua kuondoa kusudio hilo baada ya majadiliano na maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ndugu viongozi wenzangu, naomba kuwataarifu kuwa baada ya mashauriano na maelekezo ya viongozi wa juu wa CCM na hali ya kisiasa katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu binafsi ya ukomo wa Bunge niliyokusudia kuiwasilisha katika Bunge lijalo (linaloanza Novemba, mwaka huu,” aliandika Nkamia.

Hoja ya Nkamia ilianzia Bunge lililopita lakini ilipingwa na wanasiasa wakongwe akiwamo Spika Mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa na wasomi mbalimbali.

Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam, Alhamisi wiki hii, Msekwa alisema CCM haiwezi kukubaliana na maoni ya kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kwa mujibu wa Katiba ya sasa.

Pia alisema kwa uzoefu wake bungeni anaona kuna tafakuri nyingi zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alimpinga huku akisema lengo la Nkamia lilikuwa ni kujipendekeza kwa Rais Dk. John Magufuli ili ampe uwaziri.

Pia Septemba 18, mwaka huu, Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche, alisema anakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili kupunguza muda wa viongozi kukaa madarakani kutoka miaka mitano na iwe minne kama Marekani ili kutoa nafasi kwa wananchi kuwa na uamuzi zaidi wa kuendesha nchi yao.


Waziri: Nakusudia Kupeleka muswada Bungeni Maprofesa wastaafu wakiwa na miaka 65

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema ana mpango wa kupeleka bungeni maombi ya kuongezwa muda wa kustaafu maprofesa.

Amesema umri wa kustaafu kwa sheria unawafanya wasomi hao washindwe kutumika vizuri kulijenga Taifa, hivyo ataomba wastaafu wakiwa na umri wa miaka 65 badala ya 55.

Mkuchika amesema hayo leo Jumatatu Oktoba 16, alipotembelea ofisi za Sekretarieti ya Ajira na kukutana na watendaji wa taasisi hiyo.

Amesema baadhi ya kada ambazo zinafanyiwa kazi na maprofesa zinatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tofauti.

Waziri amesema wengi wanapata  uprofesa wakiwa na miaka 55 na hufanya kazi kwa miaka michache na kutakiwa kustaafu.

"Tutapeleka bungeni maombi kuwe na mabadiliko kidogo katika baadhi ya maeneo, hawa maprofesa wengi wanaofikia hatua hiyo wanakuwa na miaka kuanzia 50 na kuendelea halafu anafanya kazi kidogo anatakiwa kustaafu," amesema.

Amesema haitakuwa na maana kama wasomi hao wanatumia rasilimali za Taifa kufikia hatua hiyo halafu baada ya kuhitimu wanafanya kazi kwa muda mfupi na kutakiwa kustaafu.

Mkuchika amesema pia atawasilisha maeneo mengine ambayo yana upungufu unaotokana na sheria.

Amesema hayo akijibu changamoto iliyotolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Xavier Daudi ambaye ameeleza kuwa sheria inatoa mwanya kwa taasisi nyingine za umma kuajiri bila kupitia sekretarieti hiyo.

"Kuna mgongano wa kisheria kati ya sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira na baadhi ya taasisi za umma ambazo nazo zina mamlaka ya kuajiri watumishi kwenye taasisi zao," amesema Daudi.

Akijibu hilo, Mkuchika amesema, "Naahidi katika kipindi changu cha uwaziri nitafanyia kazi changamoto hiyo na ikiwezekana maeneo yote yawekwe sawa kisheria."

Mkuchika amewaasa watendaji wa taasisi hiyo kujiweka mbali na vitendo vya rushwa.

"Fanyeni kazi bila upendeleo, jiwekeni mbali na rushwa natambua hakuna sehemu yenye changamoto ya rushwa kama Sekretarieti ya Ajira. Usiombe faili lako lije kwangu eti mfanyakazi wa sekretarieti ya ajira ana kesi ya rushwa," amesema.

Waziri amesema, "Nitasimamia utendaji wa watumishi wa umma, tufanye kazi kulingana na malipo tunayolipwa na kodi za Watanzania. Nafahamu wapo watumishi wa umma ambao wanalipwa mshahara ilhali hawafanyi kazi inavyostahili."

Kuhusu watumishi wa umma walioshiriki na kushinda katika uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema watawashughulikia kulingana na mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Amesema wakati nchi inaingia kwenye mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa mwongozo ambao ulielekeza kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma kulingana na nafasi zao wapo wanaoruhusiwa na wasioruhusiwa kushiriki kwenye siasa.


Picha: Madarasa haya Yaliyojengwa na Deo Filikunjombe Mhhhhhh.......!!!

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe Marehemu Deo Filikunjombe ameendelea kuacha simanzi jimboni mwake kutokana na mambo mazuri aliyoyatenda jimboni humo hasa pale wanapoviona vitu alivyovifanya na kuviacha

Miongoni mwa hilo ni kujenga madarasa matatu ya aina yake katika shule ya Msingi Ludewa, madarasa ambayo hayapo sehemu nyingine katika jimbo hilo, lakini pia ni mazuri kuliko hata ofisi za walimu

Hali hiyo imedhihirishwa na muonekano wa majengo hayo ambayo yameshuhudiwa na mtandao huu na hapa chini nimekuwekea picha zake
 Muonekano wa mbele wa madarasa matatu yaliyojengwa na Deo Filikunjombe enzi za Uhai wake

 Madawati yaliyopo ndani ya madarasa hayo
 moja ya chumba cha darasa kilichojengwa na Marehemu Deo Filikunjombe enzi za uhai wake
 Ofisi ya mwalimu Mkuu inayoonekana

 Madarasa haya yaliyjengwa kwa kiwango cha hali ya juu


 Sehemu ya madarasa mengine katika shule hiyo
 majengo ya zamani ya shule hiyo ambayo yanatumika kama madarasa hivi sasa
 Darasa la zamani nalo lilipatiwa madawati ya kisasa"Watanzania vumilieni haya yatapita". - Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka watanzania kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho nchi inajitahidi kujikwamua kiuchumi

Rais magufuli ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, zilizofanyika katika uwanja wa Amani Zanzibar.
Kwenye hotuba hiyo Rais Magufuli amesema nchi yoyote inyopitia mabadiliko ya kiuchumi, ni kawaida kupitia kwenye wakati mgumu hivyo watanzania ni vyema wakawa na uvumilivu na subira, ili kuingoja neema itakayokuja.
"Licha ya ukweli kutokana na hatua tunazozichukua za kuwabana mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma, wapo wananchi wa kawaida ambao si wezi wala mafisadi wanaoathirika, hili ninalifahamu, lakini kama kweli tunataka kupambana na wizi na ubadhirifu pamoja na kuleta maendeleo kwa nchi yetu, athari hizi hatuwezi kuzikwepa, mabadiliko ya aina yoyote ile lazima yana athari kama hizi, lakini jambo la kututia moyo ni kwamba athari hizi mara nyingi ni za kipinzdi kifupi", amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameendelea kwa kusema kwamba ..."Mabadiliko ni magumu mwanzoni, yatakuwa machungu yanapofikia katikati, lakini mwishoni matokeo yake ni mazuri au ni matamu, hivyo nawaomba wananchi na watanzania tuvumile katika kipindi hichi cha mpito, baada ya muda mfupi mambo yatakuwa mazuri, lakini hata kama hayatakuwa mazuri hivi karibuni, watoto na wajukuu zetu watanufaika, na huo ndio uzalendo".
Pamoja na hayo Rais Magufuli amesitiza kwamba uchumi wa nchi unaendelea kukua, na kwamba wanaosema hivyo ni waongo na wazushi, na kuwataka watanzania wawapuuze.


Mrisho Gambo amtuliza Lema

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, amemtoa wasi wasi mbunge wa jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema, juu ya hofu ambayo amehisi anayo, kwamba anatengeneza mazingira ya kugombea ubunge wa jimbo hilo

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkoani Arusha, Mrisho Gambo amesema hofu anayopata Lema juu yake hapaswi kuwa nayo, kwani hana mpango wa kugombea nafasi hiyo, isipokuwa yeye anatekeleza majukumu yake kama mkuu wa mkoa kwa wananchi wake, huku akimtaka Godbless Lema kutekeleza majukumu yake kwa wananchi, na sio kuleta porojo ambazo wananchi hawazihitaji kwa sasa.
“Godbles Lema, akipita kwenye ziara zake nyingi badala ya kuzungumza maendeleo ya watu wetu, anazungumza kwamba mkuu wa mkoa msione anafanya hivi, kwa sababu anataka ubunge, mi nikisikia hivyo najua ana hofu, amejipima pima akaona pengine kivuli changu kinamtisha, mwambieni aache uoga, mi ni mkuu wa mkoa ambaye halmashauri zote, wabunge wote wapo chini yangu, sijawahi kuwa na wazo tofauti na kazi hii ninayofanya sasa, mwambie tu ahangaike na shida za watu asinihofie mimi”, amesema Mrisho Gambo.
Mrisho Gambo ameendelea kwa kushauri watu wa namna hiyo waache ujanja ujanja, kwani wananchi sasa hivi hawataki usanii.


Rais Magufuli: Sifuti mwenge wa Uhuru

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema hatafuta Mwenge wa Uhuru katika kipindi chake cha uongozi kwasababu una faida mbalimbali kwa taifa

Hayo ameyasema kwenye hotuba yake wakati akihitimisha mbio za Mwenge mwaka huu sambamba na kuazimisha miaka 18 ya kifo cha Baba wa Taifa kwenye sherehe zilizofanyika kwenye uwanja wa Amani Zanzibar.
Rais Magufuli amesema kwenye awamu yake kamwe hatafuta mbio hizo kwani zina saidia kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo nchini pamoja na kumuenzi Baba wa taifa Hayati Mwalimu Nyerere ambaye ndiye muasisi wa Mwenge wa Uhuru.
“Nafahamu kuna watu wanataka mbio za Mwenge zifutwe kwa kisingizio cha gharama lakini wanasahau kuwa Mwenge huo unasaidia kuanzishwa na kukamilika kwa Miradi ya maendeleo nchini. Nataka niwahakikishie kuwa kwenye uongozi wangu na Dkt. Shein hatutafuta Mwenge wa Uhuru”, amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa mbio za Mwenge zimekuwa zikisaidia kubaini madudu mbalimbali yanayofanyika kwenye Halmashauri nchini ikiwemo Miradi hewa. Rais ameahidi kuipitia ripoti nzima ya mbio hizo na kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyoainisha.


Rais Magufuli amtumbua Balozi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Oktoba 16, 2017 ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi ya Kilimanjaro Airports Development Company (KADCO), Balozi Hassan Gumbo.


Kwa taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Leonard Chamuriho imesema kuwa Rais Magufuli amemteua Gregory George Teu kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Kilimanjaro Airports Development Company (KADCO).
Mbali na hilo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa naye ametengua uteuzi wa mjumbe wa bodi hiyo Bw. Suleiman Suleiman kuanzia leo. 


Picha 21 za Kilichotokea kwenye Kaburi la Deo Filikunjombe Ludewa

Jana Oktoba 15 imetimia miaka miwili Tangu aliyekuwa Mbunge wa Ludewa marehemu Deo Filikunjombe afariki dunia kwa ajali ya Helkopta

Waandishi wa habari kutoka chama cha waandishi wa habari mkoa wa Njombe (NPC) ni miongoni mwa waliofika kwenye kaburi la Marehemu Deo na kuungana na familia ya Marehemu kufanya sala

Ikumbukwe enzi za uhai wake marehemu Deo Filikunjombe alikuwa mlezi wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Njombe

Hapa chini nimekuwekea picha za tukio hilo:- Mdogo wa marehemu Deo Filikunjombe Dkt Philipo Filikunjombe (kulia) akiwa kwenye kaburi la kaka yake Sehemu ya waandishi wa habari kutoka Njombe Press Club wakiwa na ndugu na jamaa wa familia ya aliyewahi kuwa mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe kusali katika kaburi la mbunge huyo


 
© Copyright EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog | Designed By www.peruzibongo.com